Handeni yawakaribisha Watanzania Tamasha la Utamaduni



MRATIBU wa Tamasha la Utamaduni wilayani Handeni, mkoani Tanga, Kambi Mbwana, amesema kwamba tamasha lao haliwahusu watu wa Handeni tu, badala yake juhudi zinafanyika kupata watu mbalimbali, wakiwamo kutoka wilaya za Korogwe ili kuleta picha ya kimkoa.

Tamasha hilo lililoanza kugusa hisia za wengi limepangwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu huku likiwa na lengo la kutangaza utamaduni wilayani humo na Tanzania kwa ujumla.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mratibu Mkuu wa tamasha hilo, Mbwana, alisema mbali na vikundi vya Handeni, pia itakuwa jambo la busara kama watapata washiriki wengine nje ya wilaya hiyo kwa ajili ya kuleta mvuto zaidi.
Alisema wasanii waliokuwa katika wilaya Korogwe, Kilindi na kwingineko katika mkoa huo wa Tanga, ni jambo la muhimu kuwakusanya pamoja kwa ajili ya tukio hilo.
“Itakuwa ajabu kama tunapozungumzia utamaduni wa Handeni, tutawaacha nyuma wenzetu wa Kilindi ukizingatia kuwa awali walikuwapo wilaya moja, hivyo kuna umuhimu kushirikiana nao.
“Kuna vikundi vizuri ambavyo tunatarajia tutakuwa navyo kutoka katika wilaya hizo, ukizingatia kuwa lengo letu ni zuri na hakuna sababu ya kujitenga katika mambo haya ya kimaendeleo,” alisema.
Wadhamini waliothibitisha kushiriki katika tamasha hilo ni pamoja na Phed Trans inayomilikiwa na Yusuphed Mhandeni, Grace Products, Screen Masters, Dullah Tiles $ Construction Ltd, Katomu Solar Specialist na Country Business Directory (CBD).
Wengine ni duka la mavazi la Chichi Local Ware, SmartMind & Partners chini ya ANESA COMPANY LIMITED, ikidhamini kwa kupitia kitabu cha ‘NI WAKATI WAKO WA KUNG’AA, Screen Masters, Saluti5.com, Lukaza Blog, Kajunason Blog, Jiachie Blog na Taifa Letu Blog.

Post a Comment